Friday, February 3, 2017



MTUMISHI WA MUNGU ALIYE HAI MTUME KIJANA BASHANDO AELEZEA KUHUSIANA NA UDADISI WAKE.
Mtumishi wa Mungu Bashando ni kijana wa makamo ambae amekuwa na mtazamo tofauti kidogo na Wakristo wengi, jambo linalofanya wachungaji wengi, mitume, manabii, wainjilisti, wamtazame katika jicho la machare na kuhisi kama anatumikia imani nyingine.
Mtumishi huyu ambae amezaliwa kwenye familia ya mitala huku kwa mama akiwa ni mtoto wa saba, na kwa baba akiwa ni mtoto wa nane, amekuwa na changamoto nyingi sana tangia akiwa mdogo kutokana na na tabia yake ya udadisi. "Tangu nikiwa mdogo sikuwa napenda kuona jambo nisilolijua na kuliacha pasipo kutafuta maana yake" alisema Mtume Bashando. 
Tabia yake ya udadisi imemsababisha kwenye maisha yake ajaribu mambo mengi ili kutaka kujua kuna nini kinachopatikana ndani.
Mtume Bashando amesema, siku moja akiwa mdogo mama yake mzazi Winfrida Mtalingi Challa alikuwa akisukwa nywele na shangazi yake na wakati wanaendelea na shughuli hiyo walimtuma chumbani aende kuchukua mafuta, kwa  kuwa chumba kilikuwa kimefungwa na kufuli alianza kufikilia na kujiuliza, ni kwanini mlango ufungwe na kufuli alafu ufunguo utolewe? Kwa hiyo alipofika ndani akafungua mlango na kuchukua mafuta, kisha akachomoa ufunguo kwenye kufuli akauweka mezani alafu akatoka na kufuli peke yake kisha akafunga mlango. Udadisi huo ulimtesa sana mama na shangazi yake, ikabidi shughuli ya ususi isimame kwa muda waanze kuhangaika, hadi walipofanikiwa kuchomoa funguo ndani. Baada ya kuona hali hiyo imempa mateso mama yake moyo wake ulijawa na simanzi na akaanza kujutia maamuzi yake.
Mtume Bashando anasema tangu nikiwa mdogo nimekuwa na hali ya kupenda kujiuliza mambo na kutaka kujifunza kwa vitendo lakini mara nyingi udadisi wangu umekuwa ukiniletea matokeo mabaya.
Pamoja na kupata matokeo mabaya lakini amekuwa akijua mambo mengi sana hivyo kujikuta akiwa mwalimu mzuri tangu akiwa mtoto. Mnamo mwaka 2011 Mtume Bashando alijiunga na mitandao ya kijamii, na akawa anafundisha sana kuhusiana na neno la Mungu, lakini baadae mwaka 2013 Mtume Bashando alibadilika na kuanza kuandika post za ajabu zenye kuleta changamoto ambayo badala ya watu kujadili wengine waliishia kumtukana, ama kutukanana wenyewe kwa wenyewe, huku wengine wakihoji ukristo wake na kumfananisha na muislamu ama mtu ambae hajaokoka, jambo ambalo lilimpatia umaarufu lakini kwa sehemu kubwa lilimchafua kwa watu wenye upeo mdogo ambao hawajui kudadisi ili kutafuta ukweli.
Mwishoni mwa mwaka 2016 Mtume Bashando aliibuka na nickname ya (SAW) jambo lililoonyesha kuwaudhi waislamu wengi na kuona kama amekipora cheo cha mtume Muhamad, lakini wapo baadhi waliompigia simu na kuongea nae kisha akajifunza mengi sana kutoka kwao, na kisha akawafundisha mengi kutoka kwake na hadi leo hii wamekuwa marafiki.
Mtume Kijana hadi sasa anasema katika udadisi wake wa mambo amegundua kuwa asilimia kubwa ya wakristo wanaojiita wamezaliwa mara ya pili ni watu wanaohitaji elimu ya hali ya juu, kwa maana wao hawajui kujadiri hoja, sana sana ni watu wa kulazimisha watu waamini wanachokiamini wao na endapo ukionyesha kuwa kinyume nao wanaanza kutoa lugha chafu.
Huyo ndio Mtume Kijana, mtumishi anaelitikisa anga katika kipindi hichi tulicho nacho, Mtume Kijana sasa hivi amekuwa busy sana na huduma kwani ana miariko mingi ya kuhubili nnje ya bara la Afrika ndio maana kwa sasa haonekani sana kwenye huduma nyingi za hapa nyumbani.

Saturday, January 28, 2017

BAADA YA UKIMYA MREFU PETER BANZI AAHIDI KURUDI KWA KISHINDO

Mwanamuziki wa nyimbo za Injili Peter Banzi baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu ameamua kuibuka na kusema kuwa alikuwa anatafuta utulivu ili awe karibu zaidi na Mungu. Mtumishi wa Mungu Peter Banzi ambaye alitamba kwa kibao chake Utukufu wako Baba chukua, Upako download na vingine vingi, amesema hivi sasa amerudi akiwa sio muimbaji pekee bali ni muhubili wa injili.

Peter Banzi ambae ana huduma yake ya kuwahubilia vijana wa mitaani pamoja wale walioathiliwa na madawa ya kulevya amesema kuwa wito wake sio kuimba tu bali ni kuwafikia walioko gizani na kuwafikishia nuru ya Kristo. Itakuwa haina maana nije kanisani jumapili na kuimba nikashangiliwa na kuuza cd tu wakati kuna wana kitaani wamepoteza, na hakuna wa kuwaondoa katika shimo walilodumbukia, alisema Peter Banzi. 

Mbali na yote hayo Peter Banzi ni mume na baba wa mtoto mmoja, hivyo anasema muziki wake inabidi aufanye kiutu uzima zaidi.

Sisi kama Makamanda, tunamtakia kila la kheri Mtumishi Peter Banzi.



MTUME KIJANA BASHANDO AFUNDISHA KUHUSU SIRI YA KUFANIKIWA

Mtumishi wa Mungu Mtume Bashando amefunguka na kufundisha kuwa siri ya kufanikiwa katika jambo lolote ipo katika kushinda. Mtume huyu ambae amejipatia umaarufu sana kupitia mitandao ya kijamii amefundisha kuwa, kuzaliwa kwako tu ilikubidi ushinde mbegu zaidi ya milioni zilizotoka kwa baba na kuingia kwenye ovary ya mama. Hivyo kila mtu unaemuona akiwa hai jua alishinda ndio maana akazaliwa. Mtume Bashando (SAW) amesema, dunia ni sehemu iliyojaa washindi, na ili uweze kufanikiwa katika dunia hii ni lazima uwashinde washindi uliokutana nao hapa duniani. Ukiona fitina, chuki, majungu, vijicho hiyo ni dalili ya kushindana na kushindwa, na mara zote aliyeshinda ndio huwa anarushiwa majungu kama adhabu ya kumvunja moyo. Tunashindana kila siku na hatupaswi kufa moyo, maana usiposhinda utatumika chini ya mtu aliyekushinda. Mtume Kijana Bashando (SAW) amemaliza kwa kusema, ni vigumu sana kushinda kama haujafauru kujishinda mwenyewe nafsi yako. Ushindi wa kweli uko ndani ya mtu, na kushindwa pia ni kitu kinachotoka ndani ya mtu. Wanaoshinda hawaogopi wala hawana nidhamu ya woga, na wanaoshindwa ni waoga namba moja ambao wanaogopa kila kitu. Lakini kumtambua muoga au jasiri kunahitaji hekima, jasiri sio mtu anaesimama na kupiga kelele kuwa haogopi, muoga ndio ana sifa ya kuongea, lakini jasiri ni mkimya na kila akitoka kazi ndio inayoonekana zaidi ya maneno. Hiyo ni nukuu kutoka kwa baba yetu, Mtume Kijana Bashando (SAW)


Sunday, June 28, 2015

JINSI UAMINIFU UNAVYOWEZA KUKUJENGEA HESHIMA MBELE ZA MUNGU NA MBELE ZA WATU UNAOWATUMIKIA..



Baba na mlezi wa huduma yangu ya Makamanda wa Yesu Apostle Vincent Mkalla ni miongoni mwa watumishi wa Mungu waliofanikiwa sana kiuchumi hapa Tanzania. Ninaposema amefanikiwa kiuchumi namaanisha kuwa ni tajiri sana kiasi kwamba hadi baadhi ya watu wenye upeo mdogo huwa wanamuita Freemason. Juzi jumamosi mtumishi huyunalikuwa anabatiza waongofu wapya na kuzika utu wao wa kale, Mungu akampatia neema kubwa maana katika ubatizo huo alibeba watu katika Coaster 11 ambazo zote zilikuwa zimejaza watu. Licha ya upako na mafanikio aliyo nayo lakini huyu baba ni mnyenyekevu sana, na mimi ninamiheshimu kwasababu keshapitia vita kubwa sana na Mungu akampigania hadi leo hii anaendelea na huduma. Kanisa lake liko Arusha maeneo ya Kijenge, Mwanama, linaitwa Victory Faith. Siku moja nikiwa naongea nae nilimuuliza ni nini siri ya mafanikio yake kiuchumi na kihuduma? Akanijibu kuwa ni uaminifu mbele za Mungu na kuisimamia kweli. Kisha akanipa shuhuda kuwa amewahi kupewa pesa kwa ajiri ya huduma fulani, ilikuwa ni kama shilingi million mbili hivi, na wakati huo hakuwa hata na nauri, tena yeye alikuwa anakaa Arusha na pesa hiyo alipewa wakati yuko moshi, ikambidi atembee kwa miguu toka Moshi hadi Arusha huku akiwa amezihifadhi hizo pesa za huduma bila kuchomoa hata senti tano. Na hiyo aliifanya ili kuutiisha mwili na kuufundisha moyo wake kuheshimu kila pato linalotokana na huduma ili aushinde moyo na matamanio ya uharibifu ndani ya huduma. Miaka mingi baadae Mungu akaja kumfanikisha sana kihuduma na kifedha, na pia akamfungulia milango mingi ya nnje, na kumpa marafiki wakubwa ambao ni watumishi Maarufu sana ulimwenguni. Siku moja Apostle Vincent Mkalla alihubiri kanisani hapo Victory Faith, Injili ikapenya sana mioyoni mwa watu, hadi washirika fulani matajiri mtu na mke wake wakaenda benki na kudroo shilingi million 15 Kisha wakaja kumkabidhi kama mbegu, huku wakidai kuwa ni Mungu amewaambia wampatie sadaka hiyo. Apostle Vincent Mkalla akaipokea ile pesa na kuihifadhi bila kuchomoa hata shilingi kumi. Baada ya mwezi wale washirika wakampigia simu na kumwambia kuwa mambo yao hayaendi vizuri na watoto wao wamerudishwa nyumbani baada ya kukosa ada ya shule. Apostle akawaita wale ndugu wakaenda kuonana, kisha akawauliza "Ni kwanini mumtolee Mungu alafu badala ya kubarikiwa nyinyi muingie kwenye matatizo? Wale watu wakakosa jibu, Kisha Apostle akawafundisha tofauti iliyopo kati ya kutoa kwa kusikia sauti ya Mungu na na kutoa kwa kufuata hisia baada ya kusikia Injili iliyochangamka. Baada ya hapo akawaonyesha zile pesa ambazo walizitoa, akachukua shilingi million tano na kumkabidhi baba yule kwa ajiri ya kwenda kuwalipia watoto ada, kisha baada ya hapo akamchukua kwenye gari wakaenda hadi benki na kuziingiza zile shilingi million kumi zilizobakia kwenye account yao. Ile familia ilishangazwa sana kwa uaminifu wa Apostle Vincent Mkalla na tangu siku hiyo hadi leo wamezidi kumuamini na kumuheshimu zaidi kama baba na mtumishi wa Mungu. Sasa kwa uaminifu wa namna hii kwanini Mungu asikubariki na kukuinua katika viwango vya hali ya juu!! Historia hii njema na mimi pia imeniongezea kitu katika utumishi wangu na kunifanya nimchukue mtumishi huyu kama mfano wa kuigwa. Ndiyo maana nimekushirikisha na wewe ili uweze kushiriki ushuhuda huu pamoja nami.

Friday, June 26, 2015

HAUNA HAJA YA KUWAZA SANA KUHUSU ELIMU BORA, CHAMA CHA KUSAIDIANA CHA WAFANYAKAZI WA TEGETA(CHAKUTE) KIMEKUPATIA UFUMBUZI

CHAKUTE ni chama cha kusaidiana cha wafanyakazi wa tegeta. Ofisi za chama hichi ziko tegeta. Asilimia kubwa ya wanachama wa chakute ni waalimu wa secondary ambao wengine wako kwenye ajira ya ualimu na wengine wako katika ajira nyingine tofauti na ualimu ingawa walishapita kwenye ualimu na kufanya vizuri. Wafanyakazi hawa walikaa chini na kubuni kitu ambacho kitakuwa ni msaada kwa jamii inayowazunguka na moja kati ya miradi waliamua kutumia taaluma yao ilikusaidia watanzania katika upande wa elimu.  Bila shaka kwa waliosoma Tegeta miaka ya 1999 hadi 2006 watakuwa wanamjua vyema mwalimu Steven Haule ambae alikuwa ni mwalimu katika shule hiyo, huyu pia ni miongoni mwa wanachama wa CHAKUTE ambao wameamua kubuni kitu kitakachoweza kusaidia wengi ktika upande wa elimu hususani wale wasiokuwa na uwezo mkubwa kifedha au wale waliosoma na kushindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu mbalimbali . Chakute wakishirikiana na shule ya One Nursery and Primary school sasa wanakuletea elimu bora kwa gharama nafuu. blog ya Makamanda ilipokuwa ikifanya mahojiano na wanachama hao, mmoja kati yao alisema "Malengo yetu makubwa katika chama hichi ni kusaidiana sisi kwa sisi lakini pia kusaidia jamii inayotuzunguka kama vile watoto yatima, wajane, pamoja na watanzania wengine ambao hawakubahatika kupata elimu bora kwa wakati. Na ili tuweze kutimiza malengo yetu tumeamua tuanze na shule hii ambayo ndio itakuwa msaada kwa wengi utakaowapa uhuru wa kujitegemea maana katika zama hizi hakuna urithi unaoweza kuwa bora kwa mwanadamu zaidi ya urithi wa kupata elimu, alisema mmoja kati ya wanachama wa chama cha CHAKUTE. Kazi kwako mama, baba, kaka na dada unaehitaji elimu bora au wewe ambae unahitaji mtoto wako, mdogo wako au ndugu yako apate elimu bora, nafasi ya kuchangamkia ndio hii. Njoo ufundishwe na waalimu wenye taaluma, uzoefu, pamoja na bidii katika kazi yako ili maisha yako yapate mwangaza. Shule hii ni shule inayotambuliwa kiserikli na ipo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria. Karibuni sana. Mawasiliano yetu yapo kwenye bango hapo juu.  

Wednesday, June 17, 2015

TOKEA KWENYE KUSAFISHA CHOO CHA KANISA HADI KUWA MTUMISHI BILIONAIRE.

Waswahili walisema ukistaajabu ya filauni utashangazwa na ya Musa, ama kweli wanadamu huwa hawakosi majina katika kila hali unayoipitia, ukiwa mwembamba watakuita kimbaumbau, na ukiwa mnene watakuita manyama uzembe, ili mradi tu wakupe kero na usijisikie furaha katika hali unayoipitia. Nimeanza na kuzungumza hayo kwasababu ya historia na shuhuda nzitto ninayotaka kuwaletea.
Leo nakwenda kumzungumzia Founder wa huduma ya Victory Faith, yenye makao makuu yake Arusha maeneo ya Kijenge Mwanama, anaejulikana kama Baba wa washindi Apostle Vincent Mkalla. Huyu ni mtumishi ambae Mungu anamtumia sana katika kufundisha mambo yanayohusiana na laana na jinsi ya kuziepuka. 
Kwa mara ya kwanza nimesikia historia yake toka kwa wachungaji fulani ambao walimtambulisha kwangu kama Freemason mmoja hatari sana, na nilipotaka kujua ni kwa nini wanasema hivyo au ni kitu gani kinawapa uhakika kuwa huyu ni Freemason wengi walisema huyu ni mtumishi mwenye pesa na mafanikio makubwa sana na wao hawajui pesa hizo amezitoa wapi?? Hali hii ilinisababisha nimtafute mtumishi wa Mungu huyu na kutaka kujua kama kweli yeye ni freemason kama nilivyosikia ili nijue wanafanyajefanyaje huko kwa chama cha freemason?? Story niliyokutana nayo ni tofauti kidogo na ikanifanya nikae chini na kuwaletea ukweli wa mambo.
Huyu mtumishi ni mtoto wa kipekee wa kiume na wa mwisho kwa mzee Mkalla ambae alikufa wakati yeye akiwa na siku 22 tangu azaliwe.
Katika kukua kwake historia ya baba yake kufa na aligundua kuwa aliuwawa hali ile ilimjengea uchungu moyoni na akawa amepanga kuja kulipa kisasi kwa wale waliohusika katika kifo cha baba yake. Mbali na masomo aliyoyapata lakini piaa alitumia muda wake mwingi katika kufanya mazoezi na pia kujihusisha na michezo ya kung fu ambayo ilimuwezesha hadi kuvuka hadi boda za Tanzania na kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo hayo, nchi kama vile urusi ambapo katika mchezo huo alifikia kiwango cha kutunukiwa mkanda mweusi. Hapo alikuwa ni mkristo lakini alikuwa hajaokoka na wala hajawa mtumishi bali alikuwa ni rastafari anaemiliki chuo cha karate alichokiita jina la scopion yaani nnge. 
Miaka ilienda baadae akaja kuokoka, na siku alipookoka ndani ya siku mbili alinyoa rasta zake na kuendelea na kuwa mshirika mtiifu katika kanisa na pia muhudhuriaji na muhudumu katika mikutano ya injili.Na kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafisha vyoo vya kanisa na kuhakikisha ni visafi kila wakati, kazi hiyo haikuwa na malipo ilikuwa ni kazi yake ya kujitolea na baadhi ya waumini wa kanisani wakambatiza kwa jina la kebehi la bwana mavi. Mwaka 1996 akiwa tayari ameshakomaa kwenye wokovu ndio mwaka aliofunga safari kutoka moshi na kuingia katika jiji la Arusha akiwa kamamgeni, ambapo moja kwa moja akaenda kufanya kazi ya umisionary katika kijiji kimoja cha Kimnyaki huko Meru. Huko aliweza kukutana na watumishi wa Mungu mbalimbali wakiwemo akina Askofu Ngataiti na Askofu Lyzer wa kanisa la habari maalum ambao hivi sasa ni marehemu. 
Wakati huo Apostle Vincent Mkalla hakuwa ameoa, na alikuwa ni miongoni mwa watumishi maskini sana, ambapo alikuwa amepewa hifadhi katika nyumba moja ya udongo ajihifadhi kama mtumishi, na humo ndani ya nyumba hakuwa na kitanda wala godoro bali alikuwa amemwaga mchanga mwingi chini, na ametengeneza mbao kama ile chaga, na juu ya hizo mbao ndio alikuwa analala, huku shuka yake ikiwa ni ile mifuko ya visalfeti ambayo huwa anakuja huku tz ikiwa imebeba viatu vya mitumba na mto wake ulikuwa ni biblia. Mwaka 1997 watumishi walikaa chini na kukubaliana kupinga tohara za jadi kwa wamasai baada ya kugundua wale wamasai wenye asili ya kiarusha tohara zao huwa zinaambatana na mambo mabaya ambayo ni ibada za mizimu, kwa mfano kila tohara ya hao wamasai wa asili ya kiarusha kabla ya kutahiri vijana huwa wanamuita Laibon ambae ni mganga wa kienyeji anaekwenda kwenye milima ya meru na kufukua jiwe fulani kila baada ya miaka saba na kuweka wakfu tohara hiyo huku wakiwa wanaimba nyimbo zao. Na kuna mengine mengi mabaya ambayo watumishi wa Mungu waliyabaini na kuamua kupinga tohara hiyo ambapo baadhi ya vijana wa kimasai waliafiki kutoshiriki tohara hiyo na kutaka watairiwe lakini bila muongozo wa mganga wa kienyeji Laibon, wala pasipo kuimbiwa nyimbo za kiasiri. Apostle Vincent Mkalla na mzee wake wa kanisa anaejulikana kama Ayubu ambae hivi sasa ni Mchungaji waliafiki kuwatahiri vijana hao kama walivyodai, hivyo wakachukua pesa kama shilingi laki nne kasoro na kuanza safari ya usiku kwenda kijiji cha jirani ili kuwatahiri vijana hao, wakati huo alikuwa katika mfungo wa siku 62, njiani walikutana na majambazi ambapo vijana pamoja na mchungaji Ayubu walikimbia lakini kwasababu yeye alikuwa kwenye mfungo alijikuta anaanguka chini na wale majambazi wakamkamata na kumuwekea bunduki kichwani huku wakimlazimisha atoe hela, akiwa katika kuwasikiliza jinsi alivyokuwa mchovu kwa ajili ya mfungo na koti alilovaa alisikika jambazi mmoja akisema "Achana nae huyu mzee atakuwa hana hela" na hiyo ndiyo ikawa pona yake. Alipoamka hapo aliendelea na safari ambapo mbele ndipo alikutana tena na mzee wa kanisa pamoja na wale vijana ambao walikimbia, safari yao ya kwenda kwangariba ikaendelea. walifanikiwa kufika kwa ngariba mida ya saa saba usiku na kazi ya kutahiri wale vijana ikaendelea, maana vijana walikataa kutahiriwa kimira lakini vilevile walikataa kutahiriwa kwa ganzi. Baada ya tohara hiyo walirudi kijiji cha Kimyaki ili wawarudishe kila kijana nyumbani kwao kabla ya wazee wamji kugundua kama vijana hawajatahiriwa kimira. Wakati wanarudi walifika kwenye daraja moja ambapo vijana walishindwa kuvuka ikabidi Apostle Vincent na Mchungaji Ayubu waanze kumvusha mmoja baada ya mwingine katika daraja lile, jambo la kushangaza nyuki waliwavamia na kuanza kuwang'ata kwelikweli lakini Mungu akawasaidia wakavuka salama, na mida ya saa kumi kuelekea kumi na moja walifanikiwa kufika kijijini na kumrudisha kila kijana nyumbani kwao. Baada ya wiki moja tukio lile likavuja lakini haikujulikana moja kwa moja ni nani aliyewapeleka vijana wale kwenye tohara, maana katika tohara wamasai wanakuwaga na mtu anaeitwa mdhamini, yaani mtu anaemshikilia kijana wakati wa kutahiriwa, sasa vijana wale walikamatwa na kuanza kuteswa huku wakiulizwa ni nani alikuwa mdhamini wake lakini wao wakajibu kuwa waliegamia mti, ambapo gadhabu ya wamasai wale waliielekezea kwenye mti walioelekezwa na wakaenda kuung'oa. lakini baada ya mti walianza operation ya kushughulika na wachungaji, ambapo jumanne moja Apostle Vincent alikuwa kanisani akiwa ametangaza semina, alishangaa amevamia na watu zaidi ya mia saba pale kanisani ambapo walimpiga fimbo za kutosha na wakamvunja mguu, na kuna bibi mmoja aliyekuwa muumini katika kanisa hapo alipigwa fimbo hadi akafa. Tukio hilo lilikuwa baya sana kiasi kwamba wachungaji wengine ambao walikuwa ni wenyeji wa jamii ile walikimbia na kuacha makanisa yao, wengine walikimbilia Kenya, wengine Morogoro, wengine Dodoma, huku wengi wakidhania Apostle Vincent amefariki dunia. Na kumbe Mungu alimponya na shambulizi lile lakini habari zilifika hadi kwa mama yake kuwa ameshafariki. Baada ya tukio hilo alitibiwa na akafungwa pop na akaendelea kusimama kwenye semina huku akiwa na muogo mguuni. Yeye aliendelea kumtumikia Mungu katika eneo lile ambapo jambo hilo lilisababisha hata wamasai wa jamii ile wamuhesabu kama mchungaji shujaa. Na habari hiyo ilivuma hadi kutangazwa kwenye vyombo vya habari kama vile bbc na sauti ya ujermani, hivyo ikaleta promo ya kiaina pale kijijini na kufanya semina ipete mahudhurio makubwa. Mwaka 1998 Apostle Mkalla alipata mchumba na mwaka 1999 akaoa, baada ya kuoa alikuwa amezawadiwa vyombo vya ndani na na mazagazaga kibao kama mnavyojua mambo ya harusi, lakini Mungu akamwambia jambo na akamshirikisha mke wake wakakubaliana kuchukua vitu vyao vyote na kwenda kumbariki Mchungaji mmoja ambae alikuwa anapitia katika wakati mgumu na hakuwa na vyombo vya ndani, na wao wakabakia hawana chochote kisha wakaanza kumlilia Mungu. Kweli walipita katika wakati mgumu sana wa kukosa hadi chakula lakini walidumu katika kumuamini Mungu. Baada ya muda ndio Mungu akaanza kumfungulia milango ya kihuduma na kifedha, akafunguliwa mlango wa kufaa sana katika nchi za jirani kama Kenya na UGANDA ambapo katika mikutano yake Mungu alimuinulia watu wa kusuport. Sasa wale wachungaji waliokimbia vita vya tohara baada ya kurudi na kukuta mwenzao alivumilia mateso na hakumkana Yesu wala kuiacha kazi yake ndio wlianza kuleta uvumi na maneno ya kumchafua. Zikaandikwa bbarua zikapigwa sahihi za wachungaji, zikasambazwa makanisa mengi ya Arusha kwmba huyu ndugu ni freemason, anakunywa damu za watu katika kila ajali inayotokea Arusha, wengine wakavuka hadi Kenya na kuongea kuwa akija Kenya anakuwa anaambukiza dhambi kwasababu ana watoto wengi mitaani na ameoa wake mengi, lakini hayo yote hakuyajibu bali alimkabidhi Mungu na Mungu akamjibia. Bado Mungu aliendelea kumfunguliamilango ya nnje ya nchi na kumpa kibari katika nchi kama vile SUDAN na Somalia ambapo amefungua huduma kadhaa huko. Mbali na huduma pia ni mfanya biashara, na mfugaji, na pia ana mashamba yake pamoja na nyumba kadhaa za kifahari. Ila siri ya kupata vyote hivyo ni utoaji, anaamini sana katikakutoa na pia katika kuwaheshimu masihi wa Bwana. Kwa hiyo toka katika jina la bwana mavi enzi hizo akiwa amepigika lakini leo anaitwa Freemason baada ya Mungu kumbariki. Ama kweli kila hatua unayoipiga maishani huwa inaambatana na majina yake. Sasa na mimi nimegundua kuwa hata kutukanwa na kuzushiwa pia ni sehemu ya baraka. 
Tarehe 22/23 Agosti 2015 Apostle Mkalla ambae ni mlezi wa Makamanda wa Yesu atasimama pale Landmark Hotel na kufundisha siri ya kufanikiwa, pamoja na uvumilivu wa kuwashinda waswahili na maneno yao.